Hata hivyo, urembo huu huja na hatari zake ambazo wengi wanaweza
kuzichukulia poa kwa kuwa hazitokei kwa haraka ama katika muda unaoweza
kutolewa ushahidi kwa sasa.
Moja kati ya urembo unaofanywa na wanawake wengi wa kisasa ni kuweka
kope za bandia juu ya kope halisi, kweli wengi wanakuwa na mvuto wa aina
yake wakikuangalia hasa mtoto wa kiume. Lakini hatari inayotokana na
urembo huo ni kubwa zaidi ya matokeo ya muda mfupi.
Wataalam wanaeleza kuwa kope za bandia ambazo hugundishwa kwa kutumia
gundi ya nywele inayotumika kugundisha nywele bandia kwa wenye vipara
inaweza kuwa chanzo cha upofu wa mtumiaji.
Gundi hiyo hupukutika taratibu sana kiasi cha kutoshtukiwa na kuelekea
kwenye mboni ya jicho ambayo ndio moyo wa ‘kuona’. Endapo mtumiaji
ataendelea kwa muda mrefu kutumia kope hizi bandia anaweza kujikuta
anakuwa na tatizo la kuona ama hata upofu wa haraka katika maisha yake
ya baadae.
Hata hivyo, hatari kubwa imeelekezwa kwa maduka ama vibanda vinatumia
vifaa vya bei nafuu ikiwemo gundi inayotumika. Ukwepaji wa gharama ama
kutokuwa na uwezo wa kutumia gharama kubwa kunamuingiza mrembo kwenye
hatari zaidi.
Kuwa mwangalifu, urembo usiwe chanzo cha kuhatarisha afya yako. Kumbuka Afya ni uhai wa mwili wako.